MAKHALIFA WA KIISLAM
Makhalifa Amao ni wanne wakuu:
Makhalifa Waongofu:
Baada ya kufariki Mtume (SAW) na kutoacha mtu wa kushika
mahali pake ili kuendeleza Uislamu na kuisimamisha dola yake, ilitokea haja
kubwa ya kuchaguliwa mtu wa kusimamia mambo ya Waislamu na kuiendesha nchi juu
ya misingi aliyoiweka mwenyewe Mtume (SAW), na kwa hivyo Waislamu wakashauriana
kuhusu nani atayekuwa khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe
juu yake.
Kuchaguliwa Abubakar:
Walikusanyika Maansari chini ya kipaa cha Bani Sa'ida
kushauriana kuhusu jambo hili la kumchagua khalifa wa Mtume (SAW), na akasimama
katika Maansari mkubwa wa Makhazraj Saad bin Ubada na kuwaeleza Maansari kwa
nini wao wanastahiki zaidi kuwa khalifa kutokana na wao, kwa sababu ya
kumuamini Mtume (SAW) wakati walipomkataa watu wake, na kumpokea na kumnusuru
na kupigana na maadui wa Mwenyezi Mungu mpaka ukasimama Uislamu.
Muhajirina, kwa upande wao, akiwemo Abubakar na Umar na Abu
Ubeyda, waliposikia kuwa Maansari wamekutana kujadiliana suala hili la
ukhalifa, walikwenda wakajiunga na Maansari na kuinuka Abubakar upande wa
Muhajirina na kuwaeleza watu kuwa Muhajirina ni watu wa kwanza waliomuamini
Mtume (SAW) na kupata kila aina ya mateso kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na
Mtumewe, na kukhalifu Waarabu wote ambao wakiamini ushirikina na kuabudu
masanamu, na kuwa na Mtume wao katika shida na furaha. Kisha akataja fadhila za
Maansari na kuwasifu na kuwaambia kuwa wao ni ndugu zao na hawawezi kukata
shauri bila ya wao, lakini Waarabu hawawezi kuwafuata wao kwa sababu wamezowea
kuwafuata Makureshi tangu zama za zamani na kwa hivyo viongozi hawana budi
kutokana na Makureshi, na Maansari ni mawaziri wao na washauri wao.
Akasimama Al-Hubab bin Al-Mundhir na kuwapigania watu wake
Maansari na kuwaambia kuwa nyinyi mna kila kitu, kuanzia mali na silaha na
nguvu na ujuzi wa kivita, na kuwa watu wanatazama nini mtafanya wakufuateni,
basi msikhitalifiane na kuweni kitu kimoja na hapana yeyote atakayekwenda
kinyume na nyinyi, na kwa hivyo, wakitaka atoke kiongozi kwetu na kiongozi
kwao.
Umar bin Al-Khattab akaikataa rai hii na kuwaambia kuwa
Waarabu hawatakubali wao wawe viongozi ilhali Mtume (SAW) hatokani nao, na kuwa
wao Muhajirina ni jamaa zake Mtume (SAW) na vipenzi vyake, na hapana
atakayekataa sisi tuwe viongozi baada yake.
Maneno haya hayakumridhisha Al-Hubab na akawashawishi
Maansari wasisikilize maneno ya Umar na kuwa wao ni wenye haki zaidi ya
Ukhalifa na wakiwa Muhajirina watataka kuuchukuwa kwa nguvu, basi watoeni nchi
na piganieni haki yenu, jambo ambalo lilimkasirisha sana Umar na kukakaribia
kuzuka mapigano baina ya Al-Hubab na Umar, lakini aliingilia Abu Ubeyda na
kuwaambia Maansari: Enyi jamii ya Maansari! Nyinyi mlikuwa watu wa kwanza wa
kunusuru Uislamu na kuutia nguvu, basi msiwe watu wa kwanza kubadili na
kughairi!
Kauli hii ya Abu Ubeyda iliwatuliza Maansari na kuwafanya
wafikirie maneno hayo na hoja hizo. Akasimama Bashir bin Saad katika viongozi
wa Khazraj na kusema kuwa ijapokuwa sisi tuna fadhila katika kupigana na
Washirikina na kuwa wa kwanza kuinusuru dini hii, lakini sisi hatukutaka haya
isipokuwa radhi za Mola wetu na kumtii Mtume wetu, na wala hatutaki starehe za
kidunia, kwani neema za Mwenyezi Mungu juu yetu ni nyingi, na tambueni kuwa
Muhammad (SAW) ni katika Makureshi, na watu wake ni wenye haki naye zaidi na
aula kwake kuliko sisi, na naapa kuwa Mwenyezi Mungu hataniona ninashindana nao
katika jambo hili abadan. Basi mcheni Mwenyezi Mungu wala msishindane nao.
Umar baada ya kusikia haya aliitumia fursa hii na kumwambia
Abubakar: Nyosha mkono wako ewe Abubakar! Na aliponyosha alimpa mkono na
kumchagua kuwa khalifa wa Waislamu na kumwambia: Je, hakukuamrisha Nabii ewe
Abubakar kuwasalisha Waislamu, basi wewe ndiye khalifa wa Mwenyezi Mungu na
sisi tunakuchagua wewe ili kuonyesha utiifu wetu kwa yule mbora kabisa
aliyependwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu katika sisi sote.
Akasimama Abu Ubeyda na kumuunga mkono Umar na kumchagua
Abubakar huku akisema: Hakika wewe ni mbora wa Muhajirina na wa pili aliyekuwa
na Mtume (SAW) katika pango, na mwakilishi wa Mtume (SAW) katika mambo ya dini,
basi nani huyo inayempasa kukutangulia au kutawala jambo hili badala yako?!
Kisha wote waliohudhuria hapo wakampa mkono na kumchagua
kuwa Khalifa wa Mtume (SAW) na kuonyesha utiifu wao kwake. Huu ulikuwa ni
uchaguzi wa watu maalumu kwani waliokuwepo hapo ni Masahaba wakubwa tu peke
yao. kisha siku ya pili yake alipokwenda Abubakar msikitini pamoja na Umar,
akasema Umar: Hakika Mwenyezi Mungu amelikusanya jambo lenu hili la Ukhalifa
kwa yule ambaye ni mbora wenu, sahaba wa Mtume (SAW) wa pili wake aliyekuwa
naye kwenye pango, basi simameni na muonyeshe utiifu wenu. Basi wakasimama watu
na kumchagua Abubakar.
Baada ya kuchaguliwa Abubakar kuwa Khalifa wa Waislamu,
alisimama na kusema: Ama baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume
(SAW). Enyi watu! Mimi nimechaguliwa kukutawaleni wala Mimi si mbora wenu, basi
nikifanya vizuri nisaidieni na nikifanya vibaya ninyosheni. Ukweli ni amana na
uwongo ni khiyana. Na dhaifu katika nyinyi ni mwenye nguvu kwangu mpaka
nimpatie haki yake inshallah, na mwenye nguvu katika nyinyi ni dhaifu kwangu
mpaka nichukuwe haki kutoka kwake inshallah. Asiache mmoja katika nyinyi Jihadi
katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwani watu hawaiwachi hii Jihadi isipokuwa
Mwenyezi Mungu huwapa idhlali (unyonge), wala hakuenei machafu katika watu
isipokuwa Mwenyezi Mungu huwaletea wote balaa. Nitiini maadamu nitamtii
Mwenyezi Mungu na Mtumewe, lakini nikimuasi Mwenyezi Mungu na Mtumewe basi
hapana utiifu kwenu juu yangu. Simameni msali Mwenyezi Mungu akurehemuni.
Khalifa wa kwanza: (11H-13H)
Abubakar Assiddiq alikuwa akijulikana kwa jina la
Abdul-Kaaba, kabla ya Uislamu, kisha akaitwa na Mtume (SAW) baada ya kusilimu
Abdullahi bin Abi Quhafa naye anatokana na kabila la Taym bin Murra bin Kaab
naye ni mdogo wa Mtume (SAW) kwa miaka miwili na kitu kwani alizaliwa baada ya
kuzaliwa kwa Mtume (SAW) kwa miaka miwili na miezi kidogo.
Utotoni mwake aliishi kama watoto wenzake wa hapo Makka
alipozaliwa, lakini alipokuwa kijana aliingilia mambo ya biashara akawa
ananunua na kuuza nguo na Mwenyezi Mungu akamfanikia sana katika biashara na
kuwa mmoja katika matajiri wa kubwa wa Makka.
Alisifika Abubakar toka ujana wake kuwa ni mtu mwenye
heshima kubwa na mtulivu na mpole na karimu na mwenye akili nzuri, na kwa hivyo
alikuwa hashiriki katika mambo maovu yaliyokuwa yakifanywa na watu wake hapo
Makka kama ya kulewa na mengineyo machafu, na kwa hivyo hajawahi kulewa la
katika zama za Ujahili wala za Uislamu, kama alivyoeleza bintiye Aisha.
Abubakar alikuwa akiishi katika mtaa aliokuwa akiishi
Khadija, na baada ya kuolewa Khadija na Mtume Muhammad (SAW) na kuishi katika
mtaa huo urafiki wao ulikuwa mkubwa na kuzidi kuwa na nguvu, hasa ilivyokuwa
wote wawili walikuwa ni watu wenye heshima kubwa na akhlaki njema na kujitenga
na mambo mabaya na maovu, na kushiriki katika mambo ya biashara.
Wakeze na wanawe:
Abubakar alikuwa kabla ya kusilimu ana wake wawili Umm
Rumaan na Qutayla, na baada ya kusilimu alimuoa Asmaa bint Umeys na Habiba bint
Khaarija, na watoto wake wa kiume ni AbdulRahman na Abdullahi na Muhammad na wa
kike ni Asmaa na Aisha na Umm Kulthum.
Kusilimu kwake:
Abubakar Assiddiq alikuwa ni katika watu wa kwanza kusilimu
baada ya Khadija na Ali bin Abi Talib na Zayd bin Haritha, na akashikamana sana
na Mtume (SAW) na kumuamini na kumsadiki mpaka Mtume (SAW) akampa lakabu ya
Assiddiq, na akawa katika waliobashiriwa Pepo na Mtume (SAW) na sahibu yake
wakati alipohama kwenda Madina.
Baada ya kusilimu alifanya bidii kubwa kuwavutia watu
katika Uislamu na katika watu waliosilimu kwa mwaliko wake Uthman bin Affan na
Zubeyr bin Al-Awwam na AbdulRahman bin Auf na Saad bin Abi Waqqas na Talha bin
Ubeydillah. Aidha, alinunua wengi katika watumwa na kuwawacha huru na
kuwasilimisha kama Bilal bin Rabah.
Alisimama Abubakar baada ya kusilimu kwake kumsaidia Mtume
(SAW) katika kutangaza kwake dini ya Mwenyezi Mungu tangu mwanzo wa daawa, na
aliendelea kumsaidia na kumpa moyo na kumsabilia kwa hali na mali na kuendelea
kuwa naye wakati watu walipomkadhibisha wakati wa Israa na Miraji, na kupata
nafasi ya kuhama naye wakati alipoamrishwa kuhajiri kwenda Madina na kufanya
kila lililomkinika kumsaidia mpaka kuwasili naye Madina kwa salama na amani.
Waziri wa Mtume (SAW):
Alikuwa Abubakar Assiddiq msaidizi mkubwa wa Mtume (SAW)
katika vita na amani na siku zote alikuwa naye pamoja na alikuwa ni kama waziri
wake, yeye pamoja na Umar katika kumpa mashauri mbali mbali katika mambo ya
kidunia, na alionyesha msimamo mzuri katika vita vya Uhud wakati walipokimbia
aghlabu ya Waislamu isipokuwa baadhi ya Masahaba akiwemo Abubakar, na kadhalika
katika sulhu ya Hudaybia wakati alipokubali Mtume (SAW) masharti ya Washirikina
na kukubali kurudi Madina asifanye Umra mwaka ule yakawatia dhiki sana Waislamu
haya pamoja na Umar ila Abubakar alisimama naye na kufahamu hekima ya kukubali
Mtume (SAW) masharti haya na kuwa ni ushindi kwa Waislamu.
Mwakilishi wa Mtume (SAW):
Katika mwaka wa tisa, Mtume (SAW) alimwakilisha Abubakar
kwenda na watu kuhiji huko Makka baada ya kutekwa Makka na kuwa huu ndio mwaka
wa mwisho watakaoruhusiwa Makafiri na Washirikina kuhiji hapo Makka, na
alipokuwa Mtume (SAW) ni mgonjwa na hawezi kusalisha watu alimwakilisha
Abubakar awe imamu wa watu katika Sala zao, na akawa Abubakar ndiye mtu
aliyetangulizwa na Mtume (SAW) katika mambo mbali mbali katika uhai wake, jambo
ambalo liliwafanya Masahaba kufahamu kuwa hapana anayefaa kushika Ukhalifa
isipokuwa yeye baada ya kufariki Mtume Muhammad (SAW).
Fitina ya kwanza:
Baada ya kushika Ukhalifa, alipambana Abubakar Assiddiq na
fitina kubwa iliyoenea pande mbali mbali za Arabuni na kuitetemesha dola changa
ya kiislamu, kwani baadhi ya watu walidai Utume baada ya kufa Mtume (SAW) na
kusababisha mgorogoro na mvurugano mkubwa baina ya Waislamu na makabila ya watu
hawa.
Huko Yemen alidai Aswad Al-Ansi kuwa yeye ni Mtume na kudai
kuwa anajua elimu ya mambo yaliyofichikana, na kueneza fikra zake kwenye masoko
na mahali pa biashara na kufanyia stihzai dini na kuchezea shere mafunzo yake,
na kadhalika yakafanywa haya na Maslama huko Yamama, na Talha bin Khuwaylid
karibu na Makka.
Vitendo hivi viovu vilisababisha makabila mbali mbali
yaliyokuwa na imani dhaifu kutoka katika dini na kukataa kufuata uwongozi wa
Madina na wengine kukataa kutoa Zaka, na kujikusanya mabedui na watu wa miji
mbali mbali ili kuihujumu Madina na Waislamu, jambo ambalo lilimfanya Abubakar
afanye haraka kutayarisha jeshi kupambana na fitina hii na kuukata mzizi wake
moja kwa moja.
Waislamu waliingiwa na ghera na kujikusanya kwa haraka sana
na kutoka na kiongozi wao Abubakar mpaka Dhul-Qassa, mahali Magharibi ya Madina
na kupambana na jeshi la makabila ya karibu na hapo, na baada ya kushinda
katika vita hivyo, aliligawanya jeshi lake vikosi kumi na moja na kuvipeleka
sehemu mbali mbali za karibu na mbali kupambana na uasi huu na fitina hii.
Kikosi cha kwanza kikiongozwa na Tarifa bin Hajiz
kilielekea upande wa Kaskazi-Mashariki ya Madina kwenda kupambana na Banu
Suleym na Hawazin. Cha pili kikiongozwa na Khalid bin Al-Walid kilielekea
Mashariki kuukomesha uasi wa Talha bin Khuwaylid, kisha kiende kujiunga na
kikosi cha kwanza kuwasaidia, na kikosi cha tatu kikiongozwa na Sharahbil bin
Hasana kwenda kupigana na Musaylama na kukisaidia kikosi cha Ikrima
kilichopelekwa Al-Yamama. Na cha nne kilikuwa kikosi cha Ikrima kilichopelekwa
kwa Maslama na kikosi cha tano kilipelekwa kikiwa chini wa uongozi wa Hudheyfa
bin Mahsin kwenda Diba Oman kukomesha uasi huko.
Aidha, Abubakar alipeleka kikosi cha sita kikiongozwa na
Arjafa bin Harthama kuwaendea watu wa Mahra, na cha saba kikiongozwa na
Al-Muhajir bin Umayya kumwendea Al-Aswad Al-Ansi huko Sanaa kumtia adabu na
kusitisha uasi na chengine cha nane kilipelekwa Tihama huko Yemen kikiongozwa
na Suweyd bin Muqrin, na cha tisa kikiongozwa na Al-Alaa bin Al-Hadhrami kwenda
Al-Bahrain na cha kumi ni kikosi cha Amr bin Al-Aas kwenda Kaskazini ya Bara
Arabu kuliendelea kabila la Khuzaa, na cha kumi na moja ni kikosi cha Khalid
bin Said kuelekea Mashariki ya Sham kupigana na waliortadi huko na kukisaidia
kikosi cha Amr bin Al-Aas.
Vikosi hivi vilipata ushindi mkubwa kila sehemu
vilipopelekwa isipokuwa kikosi cha Ikrima ambacho kilipelekwa kupigana na
Maslama kwa sababu Maslama alikuwa na jeshi kubwa lililokaribia watu 40,000,
lakini alipokuja Khalid kumsaidia na kikosi chake wakakimbia wale waliortadi na
ukawa ushindi ni wa Khalid. Naye Ikrima alipoona matokeo hayo alimuachia
uwongozi Khalid na yeye akaelekea Oman kupambana na Dhu Taj kiongozi wa
waliortadi huko na kumshinda kwa msaada wa Hudheyfa na Arjafa. Kisha hawa
wakaelekea Shihr na Hadhramaut na Yemen na kukomesha uasi huko. Naye Khalid
baada ya kupata ushindi alielekea Al-Bahrain kwenda kumsaidia Alaa Al-Hadhrami
ambaye alikuwa amezungukwa na maadui chini ya uwongozi wa Nuuman bin
Al-Mundhir, na kuweza kuwashinda maadui wote wa Uislamu.
Mambo muhimu aliyoyafanya:
Baada ya kuwashinda waasi waliortadi na kutoka kwenye dini
ya Mwenyezi Mungu na kuwarudisha watu katika njia ya sawa na kuikutanisha dola
chini ya utawala wa Uislamu, alifanya kila aliloweza kuipa nguvu dola ya
kiislamu na kuuhifadhi Uislamu na Sharia zake na hukumu zake.
Vita vilipomalizika, walikuwa wengi katika Masahaba
waliokuwa wamehifadhi Qurani kwa moyo walikuwa wameuliwa katika vita hivi, na
ilivyokuwa Qurani wakati wa Mtume (SAW) haikuwa imeandikwa katika kitabu kimoja
kama tunavyouona msahafu hivi leo, bali ilikuwa imeandikwa katika ngozi za
wanyama na majani ya mitende na juu ya mawe malaini na mifupa na kuhifadhiwa
kwenye nyoyo za Masahaba.
Baada ya kuuliwa Masahaba 70 wenye kuhifadhi Qurani yote
katika vita vya Yamama, alisimama Umar bin Al-Khattab kumuashiria Abubakar
hatari ya kutokusanywa Qurani Tukufu katika kitabu kimoja, lakini Abubakar
aliona uzito kufanya jambo ambalo Mtume (SAW) hakulifanya, na akasita kidogo
mpaka Mwenyezi Mungu alipoukunjua moyo wake kulikubali jambo hili. Abubakar
akamwita Zaid bin Thabit ambaye alikuwa ni mwandishi wa Wahyi wa Mtume (SAW) na
mwanachuoni mkubwa wa Qurani na mwenye kuihifadhi yote nzima ili kumtaka
aikusanye na kuiandika kwenye kitabu kimoja.
Kukusanywa kwa Qurani:
Zaid bin Thabit naye vile vile kwa upande wake alisita
kutekeleza jambo hili mpaka uzito moyoni mwake wa kufanya jambo ambalo Mtume
wake hakulifanya kumuondoka, ndipo alipowataka watu wenye maandishi ya Qurani
yoyote wayalete kwake pamoja na mashahidi wawili kuthibitisha kuwa maneno haya
yaliandikwa mbele ya Mtume (SAW), juu ya kuwa yeye mwenyewe kaihifadhi Qurani
nzima, na hii ni kwa sababu ya kuogopea kutia ndani ya Qurani maneno yasiyokuwa
ya Mwenyezi Mungu.
Qurani Tukufu baada ya kuandikwa kwenye kitabu kimoja
alikiweka Abubakar wakati wa Ukhalifa wake, kisha akakichukuwa Umar katika zama
zake na baada ya kufa Umar, msahafu ulibaki katika mikono ya Hafsa bintiye Umar
na mkewe Mtume (SAW), mpaka alipotawala Uthman Ukhalifa ndipo alipokichukua na
kufanya nuskha na kupeleka miji mengine.
Kulipeleka jeshi la Usama Sham:
Mtume (SAW) kabla ya kufariki alikuwa amemchagua Usama bin
Zayd kuongoza jeshi kwenda Sham kupigana na Warumi, lakini hakudiriki kufika
mbali, Mwenyezi Mungu akamkhitari Mtume wake na jeshi likarudi kuhudhuria
mazishi ya Mtume wao (SAW).
Aliposhika Abubakar Ukhalifa alimuamrisha Usama atoke na
jeshi lake na kuelekea Sham kwenda kupambana na Warumi, na ijapokuwa baadhi ya
Masahaba walitaka Abubakar amuuzulu Usama kwa udogo wake, kwani alikuwa wakati
huo ni kijana wa miaka kumi na saba tu, na kumpa uwongozi sahaba mwengine aliye
mkubwa, lakini Abubakar alikataa kumuuzulu mtu ambaye Mtume (SAW) mwenyewe
amemchagua, na kwa hivyo likatoka jeshi chini ya uwongozi wa Usama na kupata
ushindi mkubwa kabisa dhidi ya Warumi, na kwa hivyo akaweza kuithibitisha mipaka
ya dola ya kiislamu iliyopakana na dola ya Warumi.
Vita vya Kaadhima-12H:
Baada ya kwisha kupigana na Waislamu walioasi na kukataa
kulipa Zaka, Abubakar alimpeleka Khalid bin Al-Walid kwenda kupigana na
Wafursi, na kumuamrisha Al-Muthana bin Haritha kujiunga naye, na kwa fadhila za
Mwenyezi Mungu aliweza Khalid kushinda katika vita mbali mbali katika hivyo ni
Kaadhima au Dhatus-Salaasil, na baada ya kushinda vita hivi, Abubakar
alimuamrisha Khalid aelekee Sham kwenda kusaidia jeshi la kiislamu lililokuwa likipigana
huko.
Kutekwa Sham:
Yalipokuwa majeshi ya kiislamu yanapata ushindi huko Iraq
na Ufursi, majeshi ya kirumi yalijitayarisha huko Sham kuwahujumu Waislamu, na
kwa hivyo akatayarisha Abubakar majeshi manne kupambana na majeshi haya ya
Warumi, na kuyaamrisha yaelekee Sham.
Vita vya Yarmuk:
Wakati huu Hiraql, mfalme wa Warumi alikuwa kakusanya jeshi
kubwa sana lenye wanajeshi zaidi ya elfu mia mbili kwenda kulipiga jeshi la
Waislamu, na akampa Maahan uwongozi wa jeshi hilo.
Jeshi la Waislamu lililojikusanya karibu na mto wa Yarmuk
lilikuwa halizidi wanajeshi elfu arubaini, na alikuwa kiongozi wao mkubwa ni
Khalid bin Al-Walid, naye akamweka Abu Ubeyda bin Al-Jarrah kuongozi kikosi cha
katikati, na kwa upande wake wa kulia akamweka Amr bin Al-Aas na kikosi chake
na kwa kushotoni mwake akamweka Yazid bin Abi Sufyan na kikosi chake.
Jeshi hili lilipopambana na jeshi la Warumi lilipata
ushindi mkubwa kwa nusura ya Mwenyezi Mungu na wakashindwa Warumi na kuuliwa
kiongozi wao Maahan na wengi katika maaskari wake, jambo ambalo liliwatia moyo
sana Waislamu na kuwapa nguvu kuendelea na vita vyao dhidi ya Makafiri mpaka
wakaiteka Sham.
Nidhamu ya Uwongozi:
Wakati Mtume (SAW) alipokuwa hai, alikuwa yeye ndiye
kiongozi wa Waislamu katika mambo ya kidini na kidunia, kwani yeye ndiye
aliyekuwa mweka Sharia na hakimu na imamu na amirijeshi na mwenye kuamrisha na
mwenye kukataza.
Baada ya kufariki Mtume (SAW), walilazimika Waislamu
kutafuta kiongozi mpya atakayemwakilisha Mtume (SAW) katika mambo ya maisha,
kwani dini ilikuwa imeshakamilika na aliwachia Mtume (SAW) Qurani na Sunna ili
yawe marudio yao wakati wowote watakapohitalifiana.
Ukhalifa:
Nidhamu ya Ukhalifa au uwakilishi wa Mtume (SAW)
ilihitajika baada ya kufa Mtume (SAW) na kwa hivyo Waislamu wakarudi kwenye Qurani
na Sunna ya Mtume wao kujua nini wafanye ili wamchague Khalifa. Yakawa masharti
ambayo lazima yapatikane katika kusimamisha nidhamu hii ni:
1- Shura, yaani kushauriana Waislamu kabla ya kukata uamuzi
wowote;
2- Uaminifu, kwa yule mtu ambaye atachaguliwa kuwa ndiye
Khalifa wa Mtume (SAW) au kiongozi wa Waislamu, nao hupatikana uaminifu huu kwa
kuchaguliwa Khalifa na watu makhsusi kwanza wenye kufahamu Sharia na shuruti za
Khalifa, na kisha kukubaliwa Khalifa huyu na watu wote kwa jumla.
Sifa za Khalifa:
Khalifa au kiongozi wa Waislamu anatakikana awe na sifa
fulani ili astahiki kushika uwongozi huu, nazo ni elimu, yaani awe na maarifa
na dini ya Uislamu na hukumu za Sharia yake, na awe na uadilifu kwa kuwa mnyofu
na mwenye akhlaki na tabia njema na mwenendo mwema, na awe na uwezo wa
kuendesha na kulinda mambo ya Umma wa kiislamu kwa hekima na busara, na awe ni
mkamilifu wa akili na kiwiliwili.
Maliwali:
Tangu wakati wa Mtume (SAW), alikuwa Mtume (SAW)
akiwachagua watu kuwa viongozi wa makabila na miji fulani ili wamwakilishe
katika kusalisha watu na kukusanya Zaka, na aliposhika Abubakar aliwabakisha
Maliwali hawa katika kazi zao walizopewa na Mtume (SAW).
Ukadhi:
Aidha, Mtume (SAW) alikuwa amechagua watu fulani wenye
elimu na mambo ya dini na uadilifu kuhukumu baina ya watu wakati
wanapohasimiana na kugombana kulingana na hukumu za kisharia zinazotokana na
Qurani na Sunna za Mtume wa Mwenyezi Mungu. Aliposhika Abubakar Ukhalifa
alimchagua Umar bin Al-Khattab kuwa ndiye kadhi wake wa kuhukumu baina ya watu
kwa usawa na uadilifu na kwa kuwa Umar alikuwa ni mtu mnyofu sana na muadilifu
na mkali hataki mchezo, alikaa na kazi yake hii miaka miwili bila kujiwa na
mashtaka yoyote kutoka kwa watu.
Kufariki kwake:
Abubakar hakuishi sana baada ya kufa Mtume (SAW) kwani
ulidumu Ukhalifa wake miaka miwili na miezi mitatu na nusu, kisha Mwenyezi
Mungu akamkhitari na kufariki dunia akiwa ni mwenye umri wa miaka 63, na
kuzikwa karibu na Mtume (SAW) katika nyumba ya bintiye Aisha.
Abubakar ndiye wa kwanza...
1- Kuweka nidhamu ya Ukhalifa kwa njia ya kushauriana siyo
kwa kurithi na kuwaachia umma haki ya kuchagua Khalifa wamtakaye.
2- Kusimamisha vita dhidi ya Waislamu waliortadi na kutoka
katika dini na kufanya uasi dhidi ya dola.
3- Kukusanya Qurani Tukufu katika msahafu mmoja baada ya
kuwa imeandikwa katika sehemu mbali mbali.
4- Kupeleka majeshi kwenda kuteka nchi za Warumi na Mafursi
na kupata ushindi mkubwa.
Khalifa wa pili, 13-23H:
Aliposhikika Abubakar na kuhisi kuwa ajali yake imekaribia,
aliona bora kuwaita Masahaba na kushauriana nao kuhusu mtu atakayechukua jukumu
la Ukhalifa baada yake, naye aliashiria kuwa atakayefaa kwa kazi hii ni Umar
bin Al-Khattab, lakini baadhi ya Masahaba walihisi kuwa Umar ni mkali sana na
hana mchezo na kwa hivyo utawala wake utakuwa mgumu na mzito juu ya watu.
Pamoja na hayo Abubakar kabla ya kufariki alisisitiza na kushikilia kuwa Umar
ndiye atakayefaa kuchukua kazi hii nzito ya kuitia nguvu dola changa ya
kiislamu na kushughulikia maslaha ya umma.
Umar bin Al-Khattab:
Alizaliwa Umar Makka kabla ya vita vya Fujar kwa miaka
minne, na alikuwa ni mdogo kuliko Mtume (SAW) kwa miaka kumi na tatu, na mamake
alikuwa akiitwa Hantama, naye ni kijana anayetokana na Banu Adiy mojawapo ya
makabila ya kikureshi.
Wakeze na wanawe:
Umar katika umri wake alioa wanawake tisa nao ni: Zaynab
bint Madhuun na Umm Kulthum bint Ali bin Abi Talib na Umm Kulthum bint Jaruul
na Jamila bint Aasim na Luhayya na Umm Hakim na Fukayha na Aatika, na wanawe wa
kiume ni AbdulRahman na Abdullahi na Zayd mkubwa na Zayd mdogo na Ubeydillah na
Aasim na AbdulRahman wa kati na AbdulRahman mdogo na Iyadh. Na wanawake ni
Hafsa na Ruqayya na Fatma na Zaynab.
Kusilimu kwake:
Alisilimu Umar kwa kutakabaliwa dua ya Mtume (SAW) ambayo
aliomba kwa kusema: Ewe Mola! Upe nguvu Uislamu kwa mmojawapo wa Maumar. (Nao
ni Umar bin Al-Khattab na Amr bin Hisham). Basi Mwenyezi Mungu akamtia imani
Umar na kumhidi akasilimu baada ya kusikia ndugu yake Fatma na mumewe wanasoma
Qurani ambayo walikuwa wakisomeshwa na Khabbab. Baada ya kusoma Aya za mwanzo
za Sura ya Taha ilimwingia imani na kutaka kwenda kwa Mtume (SAW) kusilimu.
Kusilimu kwa Umar kulikuwa ni ushindi kwa Uislamu, kwani
baada ya kusilimu alidhihirisha Uislamu wake na kutaka Waislamu wajitokeze na
kudhihirisha Uislamu wao na kufanya ibada zao kweupe, na ukawa mwanzo wa
kudhihiri Uislamu, na Mtume (SAW) akampa jina la Al-Faruq, yaani Mpambanuzi
baina ya haki na batili.
Kuhamia Madina:
Umar alikuwa ni mtu shujaa sana na mshupavu na jasiri, na
alikuwa ni mkali hamuogopi mtu wala hakubali kuonewa, na kama tulivyomuona
wakati wa kusilimu kwake vipi ulikuwa msimamo wake, kadhalika wakati wa kuhamia
kwake kwenda Madina, kwani baada ya kuruhusiwa Masahaba kwenda Madina na Mtume
(SAW), aghlabu yao walitoka kwa kificho na usiku usiku kuogopa kuudhiwa na
Makureshi, lakini Umar alipotaka kwenda Madina aliuvaa upanga wake na
kuupachika upinde wake na kushika mishale yake na kuufunga kiunoni mkuki wake
na kwenda kwenye Al-Kaaba mbele ya hadhara ya Makureshi na kuizunguka Al-Kaaba
mara saba na kusali kwenye Makamu ya Ibrahim, kisha akasimama mbele ya
Makureshi na kuwaambia:
Nyuso ziharibike! Mwenyezi Mungu hazidhili isipokuwa hizi
pua (ambazo watu huziinua kwa kiburi). Mwenye kutaka kumfanya mamake akose
mwana, au mwanawe awe yatima, au mkewe awe kizuka, basi naapambane na mimi
nyuma ya hili bonde. Kisha huyo akageuka na kuelekea Madina, akiwa kila mmoja
katika waliohudhuria hapo kimya hapana aliyeweza kusema kwi!
Mambo muhimu aliyoyafanya:
Alipofariki Abubakar Assiddiq, majeshi ya kiislamu yalikuwa
kwenye mipaka ya Sham na Iraq yakipambana na Warumi na Wafursi. Aliposhika Umar
Ukhalifa lilikuwa jeshi la Abu Ubeyd Thaqafi linapambana na Wafursi lakini
lilishindwa na kuuliwa amirijeshi wao mahali paitwapo Al-Jisr. Kisha Wafursi
wakavuka daraja na kuja mpaka sehemu iitwayo Buweyb karibu na Kufa. Hapo Umar
akapeleka jeshi chini ya uwongozi wa Al-Muthana bin Haritha kwenda kuwasaidia
wenziwao Waislamu na Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa katika vita hivi vya
Buweyb mwaka wa 14H.
Vita vya Al-Qadisiya - 15H:
Baada ya ushindi wa Buweyb, Umar alitaka kuiteka Ufursi na
kutaka kwenda mwenyewe na jeshi, lakini Waislamu wakamshauri abakie Madina na
badala yake ampeleke mtu mwengine, basi akamchagua Saad bin Abi Waqqas
kuliongoza jeshi la Waislamu, na kwa hivyo katika vita vya Al-Qadisiya katika
mwaka wa 15H, aliweza Saad kwa kuwafikiwa na Mwenyezi Mungu kuwashinda Wafursi
na kumuua amirijeshi wao Rustum.
Kutekwa Madain - 16H:
Saad bin Abi Waqqas hakusita hapo kwani aliwafuata Wafursi
na kwenda katika nchi yao na kufika mpaka Madain na kuiteka baada ya kuizingira
kwa muda wa miezi miwili. Saad aliingia kumbi za majumba ya Kisra mfalme wa
Ufursi na kugeuza kuwa ni mahali pa kusali Waislamu.
Vita vya Nahawand - 21H:
Juu ya kuwa Saad aliiteka Madain, lakini alikuwa hakumpata
mfalme wao kwani alikimbia na kwenda kujikusanya na kusimamisha jeshi kubwa
kwenda kuchukua kisasi dhidi ya Waislamu. Umar akampeleka An-Nuuman bin Muqrin
kwenda kupambana na jeshi la mfalme wa Ufursi, na kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu
Waislamu waliweza kuwashinda vibaya Wafursi na kupata ushindi uliojulikana kuwa
ushindi wa shinda zote, na kwa ushindi huu Waislamu waliweza kuiteka Iraq yote
na Ufursi nzima.
Kutekwa Damaskas - 14H:
Baada ya ushindi walioupata Waislamu katika vita vya
Yarmuk, majeshi ya kiislamu chini ya uwongozi wa Abu Ubeyda bin Al-Jarrah
yalisonga kuelekea Damaskas kwenda kupambana na Warumi huko. Jeshi hili
likisaidiwa na majeshi ya Khalid bin Al-Walid na Amr bin Al-Aas na Sharahbil na
Qays yaliuzingira mji wa Damaskas siku sabiini mpaka ukasalimu amri na kutekwa
bila ya vita, na baada ya kutekwa Damaskas, ikatekwa miji mengine kama Hims na
Hamaa na Qinsirin na Laadhiqiya na Halab.
Vita vya Ajnadin - 13H:
Majeshi ya kirumi yalijikusanya Ajnadin mojawapo ya vijiji
vya Palestini baina ya Ghaza na Al-Quds na kutaka kupigana na Waislamu, lakini
jeshi la kiislamu likiongozwa na Amr bin Al-Aas liliweza kuyashinda majeshi ya
Warumi na kuteka miji mengine kama Yafa na Nablus na Aqlaan na Ar-Ramla na
A'kka na Sayda na Jubayl na Beirut.
Kutekwa Baitul-Maqdis- 16H:
Jeshi la kiislamu liliendelea kuwashinda Warumi na kuteka
miji mengine mbali mbali kama Ghaza na Nablus na Baytu Jibrin na kuendelea
mpaka likafika Baitul-Maqdis likiongozwa na Amr bin Al-Aas. Hapo Warumi
waligoma kusalimu amri, na jeshi la kiislamu likaendelea kuuzingira mji kwa
muda wa miezi minne mpaka Warumi walipoona kwamba hakuna faida ya kuushikilia
mji na kwa hivyo wakataka kufanya sulhu na wakaomba Umar mwenyewe aje kupokea
funguo za mji wa Jerusalem.
Umar alipokuja kupokea ufunguo wa mji, aliwaahidi kuwa
atawapa amani na kuandikiana nao mkataba ambao aliandika ndani yake maneno
yafuatayo:
(Haya ndiyo ya amani aliyowapa Umar kiongozi wa Waislamu
watu wa Jerusalem. Amewapa amani kwa nafsi zao na makanisa yao na misalaba yao,
na kuwa hayatakaliwa makanisa yao wala hayatavunjwa, wala hayatapunguzwa kitu
katika majenzi yake wala katika nafasi yake, wala hawatalazimishwa kuacha dini
yao wala kudhuriwa yeyote katika wao, na ni juu ya watu wa Jerusalem kutoa
jizya kama wanavyotoa watu wa Madain).
Kutekwa Misri - 18-21H:
Baada ya kumalizika kutekwa miji ya Iraq na Sham na
Palastini, Umar alimtuma Amr bin Al-Aas aelekee Misri kwenda kupambana na
Warumi huko, na baada ya kupita miji mbali mbali akiiteka na kuvishinda vikosi
vya kirumi, alifika Ain Shams na kupambana na jeshi kali hapo mpaka akataka
msaada kutoka kwa Umar, naye akampelekea jeshi la watu mia nne na lilipofika,
alijua kiongozi wa Warumi hapo kuwa hapana hila isipokuwa afanye sulhu na
Waislamu na kukubali kutoa jizya.
Kisha akaendelea Amr bin Al-Aas na jeshi lake mpaka
wakafika Alexandria ambao ndio uliokuwa mji mkuu wa Misri wa wakati huo, lakini
hakimu wa kirumi wa mji huo alikataa kusalimu amri na kwa hivyo Waislamu
wakauzingira kwa muda wa miezi minne, kisha wakaamua wauhujumu baada ya kugoma
hakimu wake kufanya sulhu, na kwa hivyo wakauteka kwa nguvu mwaka wa 21H. Juu
ya hivyo, Amr aliwapa masharti yale yale aliyokuwa akiwapa wale waliokubali
sulhu katika miji mengine, na kwa hivyo akawataka watoe jizya, naye akawapa
dhamana kuwahifadhia haki zao za ibada na kuyalinda makanisa yao na mali zao.
Maliwali wake:
Uislamu ulipoenea sehemu nyingi katika Ukhalifa wa Umar na
zikawa nchi nyingi ziko chini ya utawala wa kiislamu, aliamua Umar kuweka
maliwali ili asahilishe mas-ala ya kuhukumu nchi hizi zilizokuwa mbali na
Madina, akachagua kutokana na Masahaba wenye kujulikana kwa dini yao na ucha
Mungu wao na hekima na busara yao na elimu na ujuzi wao wa mambo ya dini na
dunia ili wawe ni wenye kuhukumu baina ya watu kwa uadilifu na wasalishe watu
na kuongoza jeshi.
Wawakilishi juu ya mali:
Aidha, aliweka Umar pamoja na Maliwali watu waliowakilishwa
kukusanya mali inayotoka katika nchi ikiwa ni Zaka au kodi za mashamba, na
walikuwa na kazi ya kuangalia kama Maliwali wanakwenda mwenendo wa sawa kama
vile vile Maliwali walikuwa wakiwatazama kama hawa Wawakilishi hawendi kinyume
na amri za Khalifa.
Makadhi:
Umar ndiye Khalifa wa kwanza ambaye aliweka Makadhi katika
wilaya mbali mbali za kiislamu, na kuwausia wafuate Kitabu cha Mwenyezi Mungu
na Sunna za Mtumewe (SAW) katika kutoa hukumu baada ya kuyachunguza mashtaka
sawa sawa, na kufanya bidii kusimamisha uadilifu na kufanya usawa baina ya
watu.
Idara 20H:
Halikadhalika, Umar ndiye Khalifa wa kwanza kuanzisha mambo
ya Idara katika zama zake, kwani aliweka sijili la kuandikia majina ya
wanajeshi na mishahara yao, na sijili ya kuandika yote yanayopatikana kutoka
wilaya mbali mbali za nchi na kuhifadhiwa katika Baytul-Maal (Hazina ya Dola),
na matumizi yake, na aliweka Baytul-Maal katika kila Wilaya ili kukusanya
mapato mbali mbali yanayopatikana katika Wilaya hizi.
Aina ya Mapato:
Katika mapato ambayo yalikuwa yakipatikana katika zama za
Makhalifa Waongofu ni haya yafuatayo:
1- Kharaji: Nayo ni
mali au mapato yanayopatikana kutokana na mashamba yaliyokuweko katika nchi
zilizotekwa kwa nguvu na vita, na kubakishwa katika mikono ya wenye nchi hizo.
2- Zaka: Nayo ni mali
inayotolewa na Waislamu Matajiri kila mwaka kusaidia Maskini na Mafakiri na
wengineo.
3- Jizya: Nayo ni
mali inayotolewa na Wadhimi (Wasiokuwa Waislamu wenye kuishi chini ya himaya ya
Dola ya kiislamu) na hutolewa na wanaume wenye uwezo katika wao.
4- Ghanima: Nayo ni
mali au ngawira inayopatikana na Waislamu kutokana na vita wanavyopigana na
wasiokuwa Waislamu.
5- Fayi: Nayo ni mali
wanayopata Waislamu bila ya vita.
6- Ushuru: Nayo ni
kodi inayokusanywa kutokana na biashara zinazofanywa na Wadhimi na wasiokuwa
Waislamu wanaofanya biashara ndani ya dola ya kiislamu, na Wadhimi hutoa nusu
ya kumi ya bidhaa na wasiokuwa Waislamu hutoa sehemu kumi ya biashara zao.
Waislamu katika zama za Makhalifa Waongofu walikuwa
wakitumia katika biashara zao pesa za kirumi (dinari ya dhahabu) na za kisasani
(dirhamu ya fedha), lakini wakitia maneno ya kiislamu kama: La ilaha illa llahu
au Muhammadun Rasuulullah.
Nidhamu ya kijeshi:
Katika zama za Mtume (SAW) na Makhalifa wake waongofu
ilikuwa nidhamu ya kijeshi ni wanajeshi wapanda farasi, na wanajeshi wa miguu,
na kikosi cha mbele, na kikosi kinachotangulia kuchunguza habari za maadui, na
warusha mishale, na mpango wao wa jeshi wakati wa vita ni kupeleka kwanza
wachunguzi wa habari za maadui, kisha wakati wa mapambano hutangulia kikosi cha
mbele na kufuatwa na cha kati na kusimama upande wa kulia kikosi na wa kushoto
kikosi.
Kikosi cha wapanda farasi ambacho ndicho kikosi kikubwa
kilikuwa kikibeba panga na mikuki na ngao na mipinde na mishale, na kikosi cha
miguu ambacho kilikuwa kikikaa nyuma ya wapanda farasi kilikuwa kikibeba panga
na ngao na kikosi kinachovitangulia vyote hivi ni kikosi cha wapanda farasi na
wanajeshi wake wanavaa vizibao vya chuma na kofia za chuma na kuchukua panga na
mikuki, na kikosi cha warusha mishale ilikuwa kazi yake kuwarushia maadui
mishale na ni kikosi kinachokusanya wanajeshi mabingwa wa kurusha mishale.
Jeshi la kiislamu lilikuwa likisifikana kwa wepesi wake wa
kukimbia na uhafifu wake kuliko majeshi ya kirumi na kifursi.
Kuanzilisha Miji:
Madina ndio iliyokuwa dola ya kwanza ya kiislamu baada ya
Mtume (SAW) kuhamia huko na kuijenga jamii ya kiislamu kwa mujibu wa Sharia na
Hukumu za Mwenyezi Mungu alizowawekea, na ndio dola iliyoendelea kuwa makao
makuu ya Makhalifa Waongofu Abubakar na Umar na Uthman.
Katika zama za Umar, na baada ya kutekwa miji mingi,
alianzisha Umar miji mipya kwa kuamrisha maamirijeshi walioiteka miji hiyo
kuijenga na kuikuza kutokana na kambi za kijeshi walizokuwa wakiishi pamoja na
famili zao.
Mji wa Basra:
Mji huu ulianzishwa na amirijeshi Utba bin Ghazawan mwaka
14H, nao ulikuwa chanzo chake ni kambi ya jeshi yenye vibanda vibanda hapa na pale,
lakini baadaye nyumba zikaanza kujengwa na makabila mbali mbali yakaanza
kuhamia kutoka sehemu mbali mbali, na haukupita muda ukawa mji mkubwa wenye
majumba na masoko na misikiti na majengo mengineo, na kuzidi idadi ya wakaazi
wake kutoka wanajeshi mia nane kufikia maelfu ya watu na famili zao. Hii ni kwa
sababu ya mahali penyewe ambapo palikuwa ni karibu na Ghuba ya Uajemi na
mapitio ya misafara ya biashara.
Mji wa Al-Kufa:
Mji huu ulianzishwa na Saad bin Abi Waqqas kwa amri ya Umar
bin Al-Khattab na kumtaka achague mahali patakapokubaliana na tabia ya ujenzi
wa kiarabu, na baada ya kuanza kama kambi ya jeshi, ulipanuka na kuimarishwa
mpaka ukawa katika miji maarufu na mikubwa ya wakati huo, na kuhamia huko wengi
katika Masahaba na Wanachuoni, katika hao ni Ibn Masuud na Ali bin Abi Talib
ambaye baadaye aliugeuza mji huu kuwa ndio mji mkuu wa dola ya kiislamu badala
ya Madina.
Mji wa Al-Fusttatt:
Mji huu ulianzishwa na Amr bin Al-Aas kwa amri ya Khalifa
Umar baada ya kuona Amr kuwa ni mahali pazuri pa kuanzisha mji kwa kuwepo maji
na kuwa karibu na jangwa linalounga mji huu na mji mkuu wa Uislamu, na baada ya
kupachagua hapa mahali alijenga msikiti na kuweka sehemu mbali mbali kwa
makabila ya kiarabu ambayo yalikuja kuhamia hapo, na kuwa kila mtaa unajulikana
kwa majina ya wanaokaa mtaa huo na likawa kila kabila lina mkubwa wao ambaye
anashughulikia mambo yao na mji ukapanuka na kuwa mkubwa na kujengwa misikiti
na masoko na mashamba na kuishi watu kwenye neema kubwa.
Halmashauri:
Kushauriana ni jambo lililohimizwa sana na Uislamu na
kuamrishwa ndani ya Qurani, kwani Mwenyezi Mungu (SW) amesema: Jambo lao ni
kushauriana baina yao. Q.
Kwa hivyo, tangu wakati wa Mtume (SAW), Waislamu walikuwa
daima wakishauriana katika mambo yao, na Mtume (SAW) mwenyewe alikuwa haamui
jambo likiwa si amri inayotokana na Mola wake bila kuwashauri Masahaba zake, na
kadhalika alifanya hivyo Abubakar zama za Ukhalifa wake, kwani akikabiliana na
mas-ala alikuwa akitazama katika Qurani, na akikosa alikuwa akitazama katika
Sunna za Mtume (SAW) na kuuliza Masahaba wenzake kama wamemsikia au kumuona
Mtume (SAW) ametoa hukumu fulani katika jambo hili au mas-ala haya, na akikosa
alikuwa akiwakusanya Masahaba na kuwashauri nini afanye.
Aidha, katika zama za Umar alikuwa akifanya kama hivi, na
alikuwa na halmashauri ambayo ilikuwa imekusanya Masahaba wakubwa na Wajuzi wa
Qurani waliokuwa wakikutanika na kuzungumzia mas-ala mbali mbali yanayowahusu
Waislamu yakiwa hayakutajwa ndani ya Qurani au Sunna ya Mtume wao (SAW), na
baada ya kujadiliana kulingana na misingi ya dini ya Uislamu, wakitoa rai yao
na Umar alikuwa akikata uamuzi wa mwisho kufuata au kutofuata kulingana na
ujuzi na maarifa aliyokuwa nayo ya dini.
Halmashauri hii ilikuwa inajadiliana mambo na mas-ala mbali
mbali katika maisha ya Waislamu yakiwa ni ya kijamii au ya kisiasa au ya
kijeshi na mengineyo, na katika mambo muhimu sana ya halmashauri hii, ni kule
kuchagua Umar watu sita kutokana nayo ili waamue nani atakayeshika Ukhalifa
baada yake na akachagua Masahaba ambao Mtume (SAW) amekufa akiwa yuko radhi
nao, nao ni Uthman bin Affan na Ali bin Talib na Talha na Zubeyr na AbdulRahman
bin Awf na Saad bin Abi Waqqas ili awe mmoja wao Khalifa baada ya kufariki
kwake na kumweka mwanawe Abdullahi bin Umar kama mshauri wao tu.
Kufariki kwake:
Baada ya kutawala Ukhalifa muda wa miaka kumi na nusu, na
alipokuwa akisali Sala ya Asubuhi, alikuja Abu Luulua Feyruz Mmajusi na
kumchoma jambia kwenye kiuno chake na baada ya siku tatu alifariki dunia.
Umar ndiye wa kwanza....
1- Kuweka Halmashauri rasmi ya kushauriana mambo ya dini na
dunia.
2- Kutoka usiku na kuchunguza hali za raia wake.
3- Kushika kiboko cha kutia adabu wenye kuasi.
4- Kukusanya Waislamu kusali Sala ya Tarawehe pamoja katika
Ramadhani.
5- Kupiga walevi mijeledi thamanini.
6- Kuupanua msikiti wa Mtume (SAW) wa Madina.
7- Kuwatoa Mayahudi Bara Arabu na kuwapeleka Sham na Iraq.
8- Kujenga miji mipya ya kiislamu nje ya Bara Arabu.
9- Kuandika juu ya pesa za kirumi na kifursi maneno ya
kiislamu.
Khalifa wa tatu: 23H-35H
Kabla ya kufariki Umar bin Al-Khattab aliwakusanya Masahaba
sita ambao anajua kuwa Mtume (SAW) amekufa akiwa yu radhi nao, nao ni Uthman na
Ali na AbdulRahman bin Awf na Talha na Az-Zubeyr na Saad bin Abi Waqqas, na
kuwataka wamchague mmoja wao ili awe Khalifa baada yake, na kuwaonya
wasipendelee jamaa zao wakichaguliwa kuwa viongozi.
Umar aliwapa siku tatu kufikia uamuzi kuhusu jambo hili, na
kuwaonya kuwa yeyote atakayeuchukuwa uwongozi kwa nguvu bila kushauriana akatwe
kichwa chake, na akamwita Abu Talha Al-Ansari akae tayari na watu khamsini
katika jamaa zake kuilinda halmashauri isiingiliwe na mtu yeyote mpaka
wapitishe uamuzi wao wa kumchagua mmoja katika wao, na wakishindwa kufikia
uamuzi, basi mwanawe Abdullahi bin Umar achague mmoja katika wao, na kama
hawakuridhia uamuzi wake, basi wawe pamoja na kundi la AbdulRahman bin Awf.
Kwa hivyo, alipofariki Umar walikutana watu hawa sita na
kujadiliana kwa muda mrefu kuhusu nani atakayekuwa Khalifa, na baada ya
majadiliano, alikubali AbdulRahman kujitoa asichaguliwe Khalifa lakini asimamie
kuchagua atakayefaa kuwa Khalifa, na walivyokuwa wengine walimchagua Ali na
wengine Uthman, na baada ya kushauriana na Masahaba wengine alitoka AbdulRahman
siku ya nne na kwenda msikitini asubuhi ambako watu chungu nzima walikuwa wamekusanyika,
na baada ya kutoa hutuba na kuwauliza watu rai zao, alisimama Saad bin Abi
Waqqas na kumhimiza AbdulRahman afanye haraka kuchagua mmoja wao kabla zogo
kuzidi ndani ya msikiti.
Hapo AbdulRahman aliuinua mkono wa Ali bin Abi Talib na
kumuuliza kama ataendesha mambo kwa mujibu wa Qurani na Sunna za Mtume (SAW),
na mwenendo wa Makhalifa wawili waliokuja baada yake, Ali akasema kuwa anatumai
kuwa atafanya, basi AbdulRahman akauacha mkono wa Ali na kuushika mkono wa
Uthman na kumuuliza kama alivyomuuliza Ali, naye akamwambia kuwa:
Inshallah ndiyo nitafanya. Basi AbdulRahman akauinua mkono
wa Uthman juu na kusema: Ewe Mola sikiliza na ushuhudie, kisha akasema: Ewe
Mola! Mimi nimejiondoshea jukumu hili kwenye shingo yangu na nimeliweka juu ya
shingo ya Uthman. Kisha akamchagua Uthman na wote waliokuwepo msikitini
wakamkubali Uthman kuwa ndiye Khalifa wao mpya.
Uthman bin Affan (47KH-35BH):
Uthman bin Affan bin Abil-Aas bin Umayya alizaliwa katika
ukoo wa kikureshi na mamake alikuwa ni Arwa bint Kureyz, naye alizaliwa katika
mji wa Taif, na alifariki babake alipokuwa anakwenda katika mojawapo ya safari
zake za Sham kwenda kuleta biashara na kumwachia mwanawe mali nyingi sana, na
akainukia kuwa mfanyibiashara mzuri na akaweza kukusanya mali nyingi na kuwa katika
matajiri wakubwa hapo Makka, na kuwasaidia watu wake mpaka wakawa wanampenda
sana na kumheshimu.
Alikuwa Uthman ni mtu karimu sana na mara nyingi alimsaidia
Mtume (SAW) kwa mali yake katika kuutangaza Uislamu na kusaidia Waislamu kama
aliponunua kisima cha Ruma kutoka kwa Myahudi ambaye alikuwa akiwatoza pesa
Waislamu kwa maji yake na kuwasabilia wateke bure na vile vile katika
kutayarisha jeshi la kwenda kupigana jihadi na mambo mengine mengi ya kusaidia
Waislamu, naye alikuwa ni mwenye haya nyingi na heshima kubwa mpaka kusema
Mtume (SAW) kuwa Malaika wanamstahi Uthman, na alikuwa akijulikana kwa jina la
Dhun-Nurayni kwa kuoa kwake watoto wawili wa Mtume (SAW) Ruqayya na baada ya
kufariki akamuoa Umm Kulthum, na ni mmoja katika Masahaba kumi waliobashiriwa
Pepo na Mtume (SAW).
Wakeze na wanawe:
Wake wote aliowaoa ni tisa nao ni Ruqayya na Umm Kulthum
watoto wa Mtume (SAW), na Naila na Faakhita na Umm Amr na Fatma na Ummul-Banin
na Ramla na Ummu Walad. Na alizaa nao watoto wa kiume na wa kike, nao ni Abdullahi
mkubwa na Abdullahi mdogo na Amr na Khalid na Abaan na Umar na Al-Walid na Said
na Al-Mughira na Abdul-Malik. Na wanawake ni Maryam na Umm Said na Aisha na Umm
Abban na Umm Amr na Maryam na Ummul-banin, wakiwa wote ni 17, wanaume ni 10 na
wanawake ni 7.
Kusilimu kwake:
Uthman alisilimu mapema baada ya Mtume (SAW) kupata utume
akiwa ni kijana mwenye umri wa miaka thalathini baada ya kuzungumziwa ujumbe
huu wa Uislamu na Abubakar Assiddiq. Naye alikuwa ni Muislamu mwema na sahaba
mkubwa katika Masahaba wa Mtume (SAW) na kuhudhuria aghlabu ya vita vya jihadi
alivyopigana Mtume (SAW), na alikuwa ni mfanyibiashara aliyepata ufanisi mkubwa
katika biashara zake.
Kuhamia kwake Habasha na Madina:
Uthman alikuwa ni katika Masahaba wa kwanza waliohamia
Habasha kwa mara ya kwanza na mara ya pili, yeye pamoja na mkewe Ruqayya binti
wa Mtume (SAW), kisha ilipotoka amri ya kuhamia Madina, akafunga safari ya
kwenda zake Madina na mkewe, na kwa hivyo amepata fadhila za kuhamia Habasha na
Madina pamoja.
Mambo muhimu aliyoyafanya:
Aliendelea Uthman kusonga mbele katika nchi mpya za
Makafiri na maadui wa Waislamu na kupigana nao na kuziteka nchi zao ili kuweka
amani kwenye mipaka ya dola ya kiislamu iliyofika sehemu mbali mbali za
ulimwengu wa wakati huo, kwani alimtuma liwali wake wa Basra Abdullahi bin
Aamir kumfuata mfalme wa Ufursi aliyewahi kukimbia katika vita vya Nahawand na
ambaye amejizatiti kupigana na Waislamu mpaka akampata na kumuua na kulishinda
jeshi lake na kuteka Karman na Sajistaan.
Aidha, katika Ukhalifa wake ilitekwa Tabaristan na Said bin
Al-Aas na kuiteka Takharistan amirijeshi mwengine aitwaye Al-Ahnaf bin Qays na
akaiteka liwali wa Uthman wa Misri, Abdullahi bin Saad bin Abi Sarh mji wa
Ifriqiya (Tunis leo) na Nuba kusini mwa Misri, na akaiteka Habib bin Maslama
miji ya Armenia, na kuwa dola ya kiislamu katika zama hizi inatawala sehemu
kubwa sana ya ulimwengu wa wakati huu.
Vile vile, aliweza Uthman kwa majeshi yake ya baharini na
majemadari wake kuviteka visiwa vya Quprus (Cyprus) na Rodz (Rhodes) na
Siqilliya (Cicily) na Kriti (Crete) katika visiwa viliopo kwenye bahari ya
Meditarenean, na kuwashinda Warumi katika vita vya Dhatas-Sawari na kuitawala
bahari yote ya Mediteranean wao.
Nuskha za Msahafu wa Uthman:
Baada ya kutekwa Armenia, Uthman alimpeleka Hudheyfa bin
Al-Yamaan kuwa liwali wake huko na kulikuwa katika jeshi lililoiteka Armenia
watu kutoka Sham na Iraq na sehemu nyenginezo na alishangazwa na kustaajabishwa
kuona watu wanakhitalifiana katika kisomo chao cha Qurani na kumueleza Uthman habari
hii ya hatari, ndipo alipokusanya Uthman maandishi ya Qurani yaliyokuwa kwenye
mifupa na ngozi na karatasi na mawe na kuchoma moto zote hizi na kuuchukuwa
msahafu ulioandikwa katika zama za Abubakar na ambao ulikuwa kwa Hafsa mkewe
Mtume (SAW) na kuamrisha ziandikwe nuskha kutokana na msahafu huu na kutawanywa
katika miji mikubwa ya kiislamu.
Kuupanua Msikiti wa Makka-29H:
Alipoona Uthman kuwa Msikiti wa Makka umekuwa hauwatoshi
Waislamu ambao idadi yao ilikuwa inazidi kila siku na kutoka kila pande za dola
ya kiislamu kubwa, alisimama kuupanua msikiti huu katika mwaka wa 29 wa Hijra.
Fitna ya pili:
Ilizuka fitna kubwa zama za Ukhalifa wa Uthman wakati watu
walipoona kuwa Uthman anapendelea watu wa kabila lake la Banu Umayya kwa kuwapa
vyeo katika miji mbali mbali ya dola ya kiislamu, na Ali bin Abi Talib
alimnasihi sana Uthman kuhusu hatari ya jambo hili, na ikawa watu wamegawanyika
mafungu matatu: Wale waliopewa vyeo na kujikusanyia mali chungu nzima na kuishi
katika anasa kwenye majumba makubwa makubwa, na wale waliokuwa wakiridhika na
kidogo na kuishi maisha yasiyokuwa na anasa na kujiepusha na starehe za
kidunia, na wale ambao walikuwa na imani dhaifu na ambao ilikuwa nia yao kutia
chokochoko na kuchochea fitna baina ya Waislamu.
Kundi la kwanza lilikuwa ni kundi la Muawiya na jamaa
wengine wa Uthman ambao walikuwa wakiishi katika hali ya juu ya maisha, na
kundi la pili ni la Ali ambalo lilikuwa likipigania watu wote wawe
wanashughulikiwa sawa sawa wasipendelewe hawa juu ya wengine, na kundi la tatu la
wachochezi fitna na wenye kutaka kuwagawanya Waislamu lililokuwa likiongozwa na
Abdullahi bin Sabaa Myahudi kutoka Sanaa aliyejidai kusilimu na kuichochea
fitna hii ambayo mwisho wake ilimpelekea Uthman kuuliwa.
Kuuliwa Uthman:
Ilivyokuwa mali katika Ukhalifa wa Uthman ilikuwa nyingi
sana na kukusanyika katika mikono ya Maliwali na viongozi wa miji na matajiri,
alisimama Abu Dhar Al-Ghafari na kuwanasihi matajiri wa hapo Madina watoe mali
zao kuwapa maskini, na kuendelea kuusia na kunasihi na kwenda huku na huko
mpaka akafika Sham na kutangaza mwito wake wa kuwaomba matajiri wawasaidie
maskini.
Mwito huu ulipomfikia Muawiya alimwita na kujadiliana
kuhusu jambo hili, lakini Abu Dhar alishikilia kuwa mali ni mali ya Waislamu na
kila mtu apewe haki yake, basi Muawiya akamwandikia Uthman amwite Abu Dhar
Madina na alipokutana naye na kumuuliza mas-ala haya, alijibu Abu Dhar kuwa
haiwapasi matajiri kuzuiya mali ya Waislamu mikononi mwao, bali inapasa watoe
kuwapa wenziwao maskini. Uthman akamwambia kuwa ni juu yake kutoa katika mali
yake tu na kuchukuwa Zaka kutokana na raiya, lakini si juu yake kuwalazimisha
kuishi maisha ya kimaskini na kujikhini. Abu Dhar akamwomba Uthman ampe ruhusa
aondoke Madina ende akaishi sehemu mbali na Madina, basi akampa ruhusa.
Kwa upande mwengine, alisimama Abdullahi bin Abi Sabaa
Myahudi aliyejidai kusilimu kutia chokochoko katika nchi alizozitembelea, nazo
ni Misri na Basra na Kufa, na kuwachochea watu wawe dhidi ya Uthman kwa hoja
kuwa hafanyi uadilifu baina ya watu na akapata wafuasi wengi, basi wakatoka
watu kutoka Basra na Kufa na Misri kwenda Madina kumtaka Uthman ajiuzulu,
lakini alipokataa Uthman kujiuzulu na kukubali kufanya matengenezo,
walikusanyika wapinzani na kuizingira nyumba ya Uthman na kumzuiya kutoka
kwenda kusali na kumnyima maji na chakula.
Wakasimama Masahaba na watoto wao akiwemo Al-Hasan bin Ali
na Ibn Abbas na Muhammad bin Talha na Abdullahi bin Zubeyr na Abdullahi bin
Salam na Marwan bin Al-Hakam na Abu Hureyra na wengi wengineo wanaokaribia watu
mia kumhami Khalifa wao, lakini waasi walikuwa wengi na baada ya kupigana na
kuumizwa baadhi ya watoto wa Masahaba, walichoma moto waasi mlango wa nyumba ya
Uthman na kuingia ndani kwa njia ya nyumba nyengine iliyokuwa imegusana na
nyumba ya Uthman na kumvamia na kumpiga na kumchoma panga na alipojaribu mkewe
Naila kumlinda walimpiga panga wakamkata vidole vyake.
Uthman aliushikilia msahafu wake na kuuweka mapajani mwake
na huku waasi wamemzunguka huyu anampiga teke, yule anamchocha jambia na
mwengine anampiga panga mpaka akaanguka na kukata roho. Masahaba walilia sana
kwa kifo chake na kiwiliwili chake kilikaa siku tatu bila kuzikwa, kisha Ali
pamoja na Talha na Masahaba wengine wakamchukuwa na kumzika.
Uthman ndiye wa kwanza...
1- Kufanya nuskha za Qurani Tukufu na kuzitawanya katika
miji ya kiislamu.
2- Kuupanua msikiti wa Makka (Al-Masjidul-Haraam).
3- Kuweka maaskari wa kulinda mji na kuwapa mishahara
wanajeshi.
4- Kuweka nyumba hasa ya kadhi ya kuhukumu baina ya watu.
5- Kujenga merikebu za vita na kuanzisha jeshi la kiislamu
la baharini.
6- Kuwapa mishahara waadhini kutokana na Baytul-Mal.
Khalifa wa nne (30H-40H):
Baada ya kuuliwa Uthman bin Affan walikutana Masahaba
wakubwa hapo Madina na kushauriana kuhusu nani atakayeshika Ukhalifa baada
yake, na wakakubaliana wamchague Ali bin Abi Talib awe ndiye Khalifa wa
Waislamu, na baada ya kuchaguliwa na Masahaba wakubwa, Waislamu wengine
wakamkubali na kuonyesha utiifu wao kwake.
Ali bin Abi Talib:
Alizaliwa Ali bin Abi Talib Makka kabla ya Utume kwa miaka kumi,
na kwa hivyo ni mdogo kuliko Mtume (SAW) kwa miaka thalathini, kwani Mtume
(SAW) wakati huo alipopewa Utume alikuwa na umri wa miaka arubaini. Mama yake
alikuwa akiitwa Fatma bint Asad bin Hashim, na kwa hivyo Ali alikuwa anatokana
na Banu Hashim kutoka kwa baba na mama, na alikuwa ndiye mdogo wa nduguze wa
kiume Talib na Aqil na Jaafar. Mtume (SAW) alimchukua Ali kumlea kwa sababu
babake alikuwa na watoto wengi na alikuwa si mtu mwenye uwezo mkubwa, na kwa
hivyo ulipoteremshwa Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Ali alikuwa akiishi na
Mtume (SAW), na kwa sababu hii akawa ni kijana wa kwanza kusilimu.
Kwa sababu ya kuishi na Mtume (SAW) na kulelewa naye,
aliinukia Ali kuwa ni kijana mwenye sifa nzuri na tabia njema na alikuwa
akijulikana kwa ufasaha wake na ukarimu wake na ushujaa wake mkubwa, kwani
inaelezwa kuwa hakupigana na mtu yeyote miereka ila alimshinda, na hakupambana
na mtu yeyote katika vita ila alimshinda na kumuua. Ali alisimama na Mtume
katika utangazaji wake wa dini ya kiislamu na alipambana na maadui wa Uislamu
katika Makafiri na Washirikina kwa ushujaa mkubwa, na unaonekana msimamo wake
huu wa ushujaa katika vita vyote alivyoshiriki, na kule kuthibiti katika vita
vya Uhud na Huneyn na kusimama kumhami Mtume (SAW) wakati Masahaba wengine walipokimbia.
Ali alihudhuria vita vyote baina ya Waislamu na Washirikina
isipokuwa vita vya Tabuk ambavyo Mtume (SAW) alimtaka abakie Madina
kumwakilisha yeye juu ya wakeze mpaka atakaporudi vitani, na alionyesha ushujaa
mkubwa kabisa na ujuzi mkubwa wa mambo ya vita wakati alipoiteka ngome ya
Mayahudi hapo Khaybar ambayo iliwashinda Masahaba wengine kuifikia. Aidha,
ushujaa na hekima yake ilidhihiri wakati alipopambana na nduguze Waislamu
ilipozuka fitna ya kuuliwa Uthman katika vita vya "Al-Jamal" na
"Siffin", na alikuwa ni mtu mwenye haiba kubwa hasa wakati wa
mapambano.
Aidha, Ali alikuwa ni katika Masahaba waliosifika kwa elimu
yao kubwa ya dini na ujuzi mkubwa wa fiqhi na hukumu za Sharia za kiislamu, na
amesimulia Hadithi 586 kutoka kwa Mtume (SAW) na kutoa fatawa nyingi ambazo
Masahaba na Makhalifa walikuwa wakizitumia katika kuhukumu na alikuwa ni
msaidizi na mshauri mkubwa wa Masahaba na Makhalifa Waongofu Abubakar na Umar
na Uthman. Vile vile alijulikana kwa ukarimu mkubwa hasa kwa watu maskini kwani
mara nyingi alikuwa akikitoa chakula chake kuwapa maskini na mafakiri na
mayatima. Naye ni katika Makhalifa wanne Waongofu na mmoja katika Masahaba kumi
waliobashiriwa Pepo na Mtume (SAW).
Wake zake:
Baada ya kumalizika vita vya Badr, alikuja Ali kwa Mtume
(SAW) kumposa bintiye Fatma, naye Mtume (SAW) alifurahi na kumpokea kwa mikono
miwili na kumuoza Fatma. Ali aliishi na Fatma peke yake mpaka akafariki na
kumzika na alizaa naye watoto wake Al-Hasan na Al-Husein na Muhsin na Zaynab na
Umm Kulthum. Aidha, alioa Ali wanawake wengine tisa baada ya kufariki Fatma nao
ni Khawla na Layla na Ummul-Banin na Ummu Walad na Asmaa na As-Sahbaa na Umama
na Umm Said na Muhayya.
Wanawe:
Mbali na watoto wa Fatma, aliruzukiwa Ali watoto wengine
kutokana na wakeze wengine nao ni, katika wanaume ni Muhammad Al-Akbar
(Ibnul-Hanifiya) na Ubeydillah na Abubakar na Al-Abbas Al-Akbar na Uthman
Al-Akbar na Jaafar Al-Akbar na Abdullah na Muhammad Al-Asghar na Yahya na Aun
na Umar Al-Akbar na Muhammad Al-Awsatt. Ama wanawe wa kike ni Ruqayya na
Ummul-Hasan na Ramla na Umm Hani na Maymuna na Zaynab As-Sughra na Ramla
As-Sughra na Ummu Kulthum As-Sughra na Fatma na Umama na Khadija na
Ummul-Kiraam na Ummu Salama na Ummu Jaafar na Jumana na Nafisa.
Hijra ya Mtume (SAW):
Alipokuwa tayari Mtume (SAW) kuhamia Madina baada ya
kuamrishwa na Mola wake kuondoka Makka, alimwita binamu yake Ali na kumwambia
alale kwenye kitanda chake kuwaonyesha Washirikina kuwa yuko Makka bado, na hii
ni kwa sababu Washirikina walikuwa wamepanga njama kutaka kumuua Mtume (SAW) na
wakawatumiza vijana wao kutokana na makabila mbali mbali ya kikureshi
kushirikiana katika kumuua Mtume (SAW) ili Banu Hashim kabila ya Mtume (SAW)
isiweze kuchukuwa kisasi.
Ali akajitolea nafsi yake na roho yake na kujisabilia kwa
ajili ya Mtume wake na kulala kwenye kitanda chake na juu ya kuwa Mtume (SAW)
alipotoka usiku ule kwenda zake kukutana na Abubakar ili waondoke kuelekea
Madina vijana wa kikureshi walikuwa nje ya nyumba wakingojea saa ya kumuingilia
Mtume (SAW) na kumuua, lakini Mwenyezi Mungu aliwafunga macho yao na kuwatia
usingizi na Mtume (SAW) akapita na kwenda zake na safari yake.
Yaliyotokea zama zake:
Baada ya kuuliwa Uthman bin Affan, alitaka Aisha akiwa na
Talha bin Ubeydillah na Az-Zubeyr bin Al-Awwam kutoka kwa Ali kuchukuwa kisasi
cha Uthman kwa wale waliomuua kwa dhulma, lakini Ali aliona ni bora kusubiri
kidogo mpaka hali ya mambo itulie nchini. Hili halikuwaridhisha Aisha na hawa
Masahaba na kwa hivyo wakaamua kuondoka Madina kwenda Makka kwa ajili ya
kufanya Umra, lakini kisha wakaelekea Basra, na ikabidi Ali atoke kuwafuata ili
kuwakinaisha kwa hoja na dalili kuacha vita na kufanya sulhu, lakini watu wa
Abdullahi bin Sabaa waliokuwa katika jeshi la Ali walileta mgorogoro kwa
kuanzisha vita na kuwahujumu kina Talha na Az-Zubeyr ili isiwepo sulhu, na
vikazuka vita vikubwa mahali paitwapo Al-Khariba karibu na Basra.
Vita vya Ngamia 36H:
Vita hivi vilijulikana kuwa ni vita vya ngamia kwa sababu
ya kuwepo Aisha mke wa Mtume (SAW) ndani ya kijumba juu ya ngamia akiongoza
vita hivi, na vita vilikuwa vikali na wengi waliuliwa kutoka pande zote mbili
akiwemo Talha na Az-Zubeyr na akakatwa miguu ngamia wa Aisha na kuanguka chini,
na ushindi ukawa wa Ali bin Abi Talib, na baada ya vita Ali akamchukua Aisha na
kumrudisha Madina kwa heshima ambako aliishi kwa amani mpaka ilipofika ajali
yake mwaka wa 58H.
Vita vya Siffin 37H:
Sababu ya vita hivi ni kuwa Ali baada ya kushika Ukhalifa
aliwauzulu maliwali wote waliowekwa na Uthman bin Affan kwa hoja ya kuwa
walikuwa wakijikusanyia mali ya umma na kuishi wao katika starehe, lakini hili
halikuwaridhisha maliwali, na Muawiya bin Abi Sufyan akiwa ni liwali wa
Damaskas aligoma kuuzuliwa na kudai pamoja jamaa zake kina Banu Umayya
kilipizwe kisasi cha kuuliwa Uthman, na kwa hivyo Ali akatoka na jeshi kwenda
kupambana naye kwa kutoka kwenye utiifu wa Khalifa na kumuasi kiongozi wa
kisharia aliyechaguliwa na umma.
Vita vilikuwa vikali sana na viliendelea muda wa siku mia
na kumi na kuuliwa idadi kubwa ya watu pande zote mbili, na likawa jeshi la Ali
linakaribia kushinda, ndipo alipojitokeza Amr bin Al-Aas ambaye alikuwa upande
wa Muawiya na kuamrisha jeshi la Muawiya liinue misahafu juu ya mikuki yao
kutaka vita visimamishwe na ipite hukumu kwa mujibu wa Qurani.
Jeshi la Ali ambalo lilikuwa limekusanya wasomi na
wahifadhi Qurani wengi sana waliikubali fikra hii na kumtaka Ali akubali
kuhukumiwa na Qurani. Ali alifahamu hila hii na aliwaonya watu wake kwa kujua
hila za Muawiya lakini wasisikie, na kwa hivyo akawakubalia.
Hila ya Amr:
Kukubali huku kwa Ali kuhukumiwa baina yake na Muawiya
kulileta mchafuko na mgawanyo mkubwa katika kundi la Ali bin Abi Talib na
kusababisha kuvunjika nguvu za Ali na kuzidi nguvu za Muawiya, kwani walipoanza
kuhukumiwa akiwa kwenye upande wa Ali, Abu Musa Al-Ash'ari na upande wa
Muawiya, Amr bin Al-Aas. Na walipokutana baina ya makundi mawili haya na
kuzungumza, waliamua kwa hila aliyoitumia Amr bin Al-Aas wawauzulu wote wawili
Ali na Muawiya na achaguliwe na Waislamu Khalifa wanayemtaka, na wakakubaliana
kuwa aanze Abu Musa kumuuzulu Ali, na baada ya kufanya hivyo, alisimama Amr na
kumthibitisha Muawiya na kumchagua yeye kuwa ndiye Khalifa na alifanya hivyo
kutokana na ahadi aliyopewa na Muawiya kuwa atampa uliwali wa Misri ambao
aliuzuliwa na Uthman wakati alipokuwa Khalifa.
Wakati jambo hili linafanyika Ali alikuwa yuko Kufa huko
Iraq anangojea hukumu ipitishwe, na kundi lake lililokuwa naye liliposikia kuwa
ameuzuliwa lilimkasirikia na kumlaumu kukubali kuhukumiwa hasa ilivyokuwa yeye
ni Khalifa wa kisheria aliyechaguliwa na Waislamu na kwa hivyo fitna mpya
ikazuka na watu katika kundi lake wakatokana naye na kuunda kundi lililokuja
kujulikana kama "Al-Khawarij" yaani wale waliotokana na Ali, na
kusababisha kundi hili balaa kubwa, kwani liliwakataa wote Ali na Muawiya na
kuanza kufanya fujo na ghasia na kupigana na akasimama Ali kuwarudisha katika
njia ya haki wasisikie ikabidi kupigana nao katika mahali paitwapo
"An-Naharawan" mpaka akawashinda na kuvunja nguvu yao.
Kuuliwa kwake 40H:
Ali alibaki Al-Kufa huko Iraq na kuufanya mji wa Al-Kufa
kuwa ndio mji mkuu wa dola ya kiislamu badala ya Madina, na kuwahimiza watu wa
Sham kupigana na Muawiya, lakini Muawiya alikuwa ni mtu mwenye siasa kubwa na
aliweza kuwatia mkononi watu wa Sham, lakini Makhawarij hawakunyamaza kwani
walipanga njama na kutuma watu watatu kwenda kuwaua Ali na Muawiya na Amr,
akapelekwa AbdulRahman bin Muljim kwenda Al-Kufa kumuua Ali, na mwengine kwenda
Sham kumuua Muawiya, na wa tatu kwenda Misri kumuua Amr.
Katika hawa watatu aliyefanikiwa kuua ni mmoja tu, kwani
yule aliyekwenda kwa Muawiya aliwahi kumjeruhi tu akakamatwa, na yule
aliyekwenda kwa Amr alimuua mtu mwengine badala ya Amr akidhani kuwa ndiye Amr,
lakini aliyetoka kumuua Ali alimwahi akiwa anatoka kwenda kusali Alfajiri siku
ya Ijumaa tarehe 17 ya Ramadhani mwaka wa 40 wa Hijra akamtia jambia la sumu na
akafariki baada kupita siku tatu akiwa amekufa shahidi.
Ali alizikwa Al-Kufa akiwa ametimiza miaka sitini na tatu
na kukaa katika Ukhalifa kwa muda wa miaka mitano, na kwa kufa yeye
zikamalizika zama za Makhalifa Waongofu ambao walikuwa wakifuata Qurani na
mwenendo wa Mtume (SAW) katika maisha yao na utawala wao.
Ali ndiye wa kwanza...
1- Kuhamisha mji mkuu wa dola ya kiislamu kutoka Madina
kuupeleka Al-Kufa huko Iraq.
Leave a Comment